Safari
za ndege za Kimataifa hatimaye zimeanza tena katika uwanja wa ndege wa
kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya kufuatia hapo jana kusitishwa kutokana
na ajali ya moto kwenye uwanja huo.
Hapo
jana Serikali ya Kenya ilitangaza kusitisha safari zote za kimataifa kwenye
uwanja huo kutokana na kuungua kwa sehemu ya uwanja hasa kwenye eneo la
kuwasili kwa abiria wa kimataifa pamoja na idara ya uhamiaji.
Ndege
nyingi hapo jana zilizokuwa zikitarajiwa kutumia uwanja huo zililazimika
kukatisha safari zao na kuelekea kwenye nchi jirani za Tanzania na Uganda huku
baadhi zikielekezwa kwenye uwanja wa kimataifa wa Moi mjini Mombasa. Rais Uhuru
Kenyatta pamoja na waziri wa masuala ya usafiri wa Kenya hapo jana waliahidi
kufanya kila linalowezekana ili kufanikisha kurejeshwa kwa safari za kimataifa
kwenye uwanja huo jambo ambalo limeanza kushuhudiwa hii leo.
Ndege
ya kwanza kutua ilikuwa ikitokea nchini Uingereza na kutua majira ya ya saa
kumi na mbili na nusu kwa saa za Afrika Mashariki. Ndege nyingine
zilizoshuhudiwa zikitua kwenye uwanja huo ni pamoja na zile zilizotoka nchini
Bangkok na kilimanjaro nchini Tanzania hali ambayo sasa inatoa matumaini ya
kurejea kwa safari nyingi hii leo.
Uwanja
wa Ndege wa Jomo Kenyatta ni uwanja mkubwa zaidi kutumika kwenye kanda hii ya
Afrika Mashariki ambapo huudumia zaidi ya abiria elfu kumi na sita kwa siku. Wataalamu
wa masuala ya uchumi wanasema kuwa kutokana na kuungua kwa sehemu ya uwanja huo
na kusitishwa kwa safari nyingi hapo jana kumeathiri kwa kiasi hali ya uchumi
wa taifa hilo kwakuwa uwanja huo umetegemewa kwa kuingiza watalii wengi zaidi.
Shughuli
za usafiri wa Tax zilikosa wateja kutokana na moto huo huku wachuuzi wa
barabarani pia nao wakidai kuathirika kutokana na ajali hiyo. Safari za ndege
za ndani zenyewe zilianza hiyo jana mara baada ya moto mkubwa kudhibitiwa. Moto
huo ulianza majira ya saa kumi za alfajiri usiku wa Jumatano na kusababisha
kuunguza sehemu kubwa ya idara ya uhamiaji na sehemu ya kuingilia abiria wa
kimataifa.
Uchunguzi
tayari umeanza kubaini chanzo cha moto huo.