Jumatatu, 26 Agosti 2013

WATU WAWILI WAPOTEZA MAISHA KATIKA MAANDAMANO HUKO GOMA

Baada ya kuawa kwa watu watu mjini Goma na makombora yaliorushwa katika mji huo wakati wa mapambano baina ya waasi wa kundi la M23 na wanajeshi wa serikali wa FARDC, wananchi mjini Goma wamepatwa na hasira na hivo kuandamana mwishoni mwa juma.Watu wawili wamepoteza maisha katika maandamano hayo. 

Umoja wa Mataifa unasema umeanzisha uchunguzi kubaini ikiwa kweli wanajeshi wake wa kulinda wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walihusika na vifo vya watu wawili mjini Goma mwishoni mwa wiki iliyopita.

Walioshuhudia mauaji hayo wanasema kuwa wanajeshi wa MONUSCO raia wa Uruguay waliwapiga risasi watu wawili wakati walipokuwa wanasambaratisha kundi la waandamanaji lililokuwa limevamia kambi ya jeshi hilo.

Mauaji haya yametokea siku moja tu baada ya kutokea kwa shambulizi la guruneti mjini Goma na kusabisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhiwa wanajeshi watatu wa kulinda amani.

Wiki iliyopita, waasi wa M 23 na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wamekuwa wakipambana karibu na mji wa Goma huku kila upande ukituhumiana kuanzisha makabiliano hayo.

Ukosefu wa amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umeilazimu serikali ya Uingereza kuwataka raia wake wote wanaoishi na kufanya kazi mjini Goma kuondoka kwa kuhofia usalama wao.

Kiongozi wa kundi la M 23 Betrand Bissimwa amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akilalamikia kuhusika kwa jeshi la kulinda amani katika mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo na kutekeleza mauaji .

Jeshi la serikali kwa upande wake linasema kuwa litaendelea kulinda mipaka ya nchi hiyo na pia kukabiliana na makundi ya waasi likiwemo la M 23 ikiwa litaanza kuwavamia.

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M 23 yamegonga mwamba jijini Kampala Uganda suala ambalo limeendelea kuhatarisha usalama Mashariki mwa nchi hiyo.