Jumanne, 6 Agosti 2013

MICHUANO YA KIKAPO YA AFRIKA MASHARIKI YATIMUA VUMBI JIJINI BUJUMBURA


Michuano ya kikapo inayojumuisha nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na kati Zone V, imezinduliwa jana jijini Bujumbura. Hii ni mara ya pili Burundi inakuwa mwenyeji wa michuano hiyo. Mechi ya kwanza ya ufunguzi imezipambanisha timu za wanawake les Gazelles ya Burundi na APR wa Rwanda, na kushuhudia le Gazelles wakiilaza APR kwa vikapo 50 kwa 35.
Mechi iliofuatia na ambayo ilikuwa ikisubiriwa na wengi ilizikutanisha timu bingwa wa michuano hiyo mwaka 2012 Espoir ya Rwanda pamoja na Urunani ya burundi ambayo iliwahi kutwaa kombe la michuano hiyo mwaka 2011. Licha ya kucheza mbele ya mashabiki wake, Urunani ililazwa na Espoir kwa vikapo 60 kwa 41
Berco Stars ambayo ilianza michuano hiyo kwa matumaini, lakini ilijikuta ikimaliza mechi kwa maskitiko. Timu ya Kenya ya USIU (United states international university) waliibuka washinda kwa vikapo 76 kwa 71. kati ya wachezaji 12 wa Kenya, wanne ni kutoka Burundi katika Mkoa wa Ngozi. Nao ni : Diane Richesse Nikuze, Ghislaine Munezero, Magnifique Ndayikengurukiye pamoja na Cynthia Kaburundi.
Mechi ya mwisho kwa siku ya jana ilizipambanisha Riham Warriors, ya Uganda na New Stars wa Burundi. Waganda ndio walikuwa wanaongoza awamu ya kwanza ya mchezo kwa vikapo 19 kwa 17 kabla ya umeme kukatika kwenye uwanja wa wizara ya michezo vijana na utamaduni.
Baada ya muda wa saa nzima hivi kabla ya shirika la maji na umeme Regideso kurejesha umeme. Timu hizo zilirejea uwanjani huku kila upande ukionyesha ushindani mzuri, lakini hata hivyo Vijana wa Uganda waliwashinda warundi kwa vikapo 93 kwa 69 huku kila upande ukionyesha mchezo mzuri.
Michuano hiyo inaendelea leo ambapo News Stars wanachuana na Vijana kutoka Tanzania.