Jumatano, 17 Julai 2013

JESHI LA DRCONGO LASEMA KUWA LIMEWASAMBARATISHA WAASI WA M23

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC limeendelea kukabiliana na wapiganaji waasi wa kundi la M23 mashariki mwa nchi hiyo siku mbili baada ya kuuawa kwa watu 130 wa kundi hilo. Msemaji wa jeshi la DRC, Kanali Olivier Hamuli amedhibitisha wanajeshi wake kukabiliana na waasi jirani na maeneo ya mji wa Goma wakati huu ambapo jeshi la nchi hiyo limeapa kuwasambaratisha wapiganaji hao.

Wanajeshi wa Congo wakielekea kwenye uwanja wa mapambano

Hayo yanajiri wakati, balozi wa DRC kwenye Umoja wa Mataifa UN ameendelea kuishutumu nchi ya Rwanda kwa kuendelea kuwafadhili kwa silaha waasi wa M23 na kuongeza kuwa wengi wa wapiganaji waliokamatwa nchini humo ni kutoka jeshi la Rwanda. Umoja wa Mataifa umevionya vikosi vyake vilivyoko mashariki mwa nchi hiyo na hasa vile vikosi maalumu vilivyopelekwa nchini humo kukabiliana na makundi ya waasi, kuwa tayari muda wote kutokana na kuendelea kushuhudiwa kwa mapigano.

Kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa kilichopelekwa nchini humo bado hakijaanza kazi yake lakini huenda kikaruhusiwa hivi karibuni kuanza operesheni ya kuwakabili waasi hao. Waasi wa M23 ambao waliwahi kuushikilia mji wa Goma kwa siku kumi mwaka jana kabla ya kuondoka kutokana na shinikizo toka jumuiya ya kimataifa lilianza tena harakati zake za kutaka kutejea kwenye mji huo na ndio chanzo cha kuzuka kwa mapigano hayo.

Msemaji wa kundi la M23 Amani Kabasha amesemalicha ya jeshi lake kuelezwa kuzidiwa na wanajeshi wa Serikali yeye ameendelea kukanusha kuuawa kwa askari wake huku akisisitiza kuwa wanayashikilia maeneo ambayo awali walikuwa wanayakalia. Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende amesisitiza jeshi la nchi hiyo kuwazidi nguvu waasi wa M23 na kwamba hivi karibuni watatangaza ushindi dhidi ya kundi hilo ambalo sasa linaelezwa kusaidiwa pia na wapiganaji wa Al-Shabab toka nchini Somali.