Hague amekiri tukio lililofanywa na wanajeshi wa Uingereza kwa kuwanyanyasa na kuwatesa wapiganaji na hata wananchi wa kawaida ambao walikuwa wanadaia uhuru wao katika kipindi cha miaka ya 1950. Serikali ya Uingereza imetangaza kuwalipa waathirika 5,228 waliopitia madhira mengi kipindi cha vita vya Mau Mau ambapo wanajeshi wa taifa hilo walivamia hadi kambi za raia wa Kenya kipindi cha vita hivyo.
London kupitia Waziri Hague imeomba radhi kama ambavyo iliahidi na kisha kutangaza fidia hiyo kutokana na kuguswa na vitendo vya mateso vilivyowakumba wananchi wa Kenya walioshiriki vita vya Mau mau. Hatua ya Serikali ya London kuomba radhi na hatimaye kulipa fidia inakuja baada ya waathiriwa hao wa vita vya Mau Mau kufungua kesi wakilalamikia utesajwi waliokumbana nao wakati wa vita hivyo.
Waathiriwa hao wa vita vya Mau Mau kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakipambana kuhakikisha wanapata fidia hiyo baada ya kutokea vita vya kudai uhuru vilivyofanyika katika miaka ya 1950.